Share news tips with us here at Hivisasa

Maduka makuu katika kaunti ya Mombasa yametakiwa yawape wakulima na wafugaji wa kaunti hiyo nafasi za kuuza bidha zao.

Akitoa mwito huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani katika eneo la Bamburi mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mkuu wa idara ya kilimo, mifugo na ustawi wa uvuvi katika kaunti hiyo Anthony Njaramba alisema kwamba maduka makuu yaliyo katika kaunti hiyo hayajawapa soko wakulima na wafugaji.

Kulingana na Njaramba, iwapo bidhaa za wafugaji pamoja na wakulima zitapata soko la tayari katika maduka makuu, basi sekta ya kilimo na ufugaji itaimarika kwa kiwango kikubwa.

"Tunataka kuona wenye maduka makuu mjini Mombasa wanawapa wakulima na wafugaji nafasi za kuuza bidhaa zao katika maduka hayo na kuendeleza shughuli za kimaendeleo ili kuona kwamba sekta hiyo inaimarika kwa asilimia kubwa,” alisema Njaramba.

Aidha, aliwahimiza wafanyibiashara wa kaunti hiyo waafikiane na serikali ya kaunti katika masuala mbali mbali yanayohusu sekta ya kilimo na ufugaji, ili kuafikia malengo yaliyowekwa.

“Tunawaomba wafanyibiashara washirikiane nasi katika maswala mbali mbali yanayohusu sekta hii ili kuona kwamba wakulima na wafugaji wanasaidika katika miradi mbalimbali inayotolewa na serikali," aliongeza Njaramba.

Kauli yake imejiri baada ya lalama kutoka kwa wakulima na wafugaji kutokana na kukosa nafasi za kuuza bidhaa zao katika maduka makuu mjini humo, pamoja na bidhaa zao kuangazia vyema na wadau wa sekta ya kilimo.