Wamiliki wa nyumba katika mitaa ya mabanda kwenye Kaunti ya Nakuru wamepewa makataa ya siku 21, kuhakikisha vyoo na mabafu ya wapangaji wao yako katika hali bora na ya viwango vya usafi vinavyostahili.
Akizungumza mjini Nakuru siku ya Jumanne, afisa wa afya katika Kaunti ya Nakuru Samuel King’ori alisema kuwa amepokea malalamishi kadhaa kutoka kwa baadhi ya wapangaji wanaoishi katika mitaa mbalimbali ya mabanda.
“Wapangaji hao wanahofia afya yao kwani kuna baadhi ya vyoo ambavyo vimejaa,” alisema King’ori.
King’ori aidha alisema ni kinyume na sheria kwa wenye nyumba kutengeneza bafu moja na choo kimoja kwa wapangaji zaidi ya ishirini katika ploti moja.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa muda huo, watazuru mitaa hiyo na wenye nyumba ambao hawatakuwa wamezingatia amri hiyo watakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kukosa kuzingatia hali ya afya wa wapangaji.