Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Utawala wa Kaunti ya Uasin Gishu umeanzisha msako dhidi ya wamiliki wa nyumba ambazo zina wapangaji ilihali hazijakamilika.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu Daniel Chemno alisema kwamba wamiliki wa nyumba hizo watachukuliwa hatua za kisheria mbali na kuwataka wapangaji katika nyumba hizo kuhama kabla ya kutiwa mbaroni.

Akihutubu wakati wa maafisa kutoka shirika la kitaifa la kukadria ubora wa mijengo walipomtembelea siku ya Ijumaa, Chemno alisema hatua hiyo inalenga kuzuia kutokea kwa mkasa wa kuporomoka kwa majumba mjini humo kama vile imekuwa ikishuhudiwa katika miji mingine haswa Nairobi.

“Hatutaki tungojee hadi pale mkasa utakapotokea ndiposa tuanza kutafuta misaada ya dharura kwa wahasiriwa. Tunataka kuzuia majanga kama hayo kutokea katika kaunti hii,” alisema Chemno.

Chemno aidha alitaka wamiliki wa mijengo ambayo maeneo ya chini ya kuegesha magari yanatumiwa kama vibanda vya biashara kubomoa vibanda hivyo.

Alisema ni kinyume cha sheria kwa sehemu ya chini ya mijengo kutumika kama nyumba za biashara ilhali maeneo hayo yanapaswa kuwa ya kuegesha magari.

Naibu gavana huyo aliwapa wamiliki husika makataa ya mwezi mmoja kuhakikisha kuwa wamebomoa mijengo hiyo ili sehemu hizo zitumike kama maeneo ya uegeshaji magari kama ilivyokusudiwa.

Kiongozi huyo alitaka wamiliki wa nyumba ambazo zina ghorofa zaidi ya nne kuhakikisha kuwa wana viinuzi na njia spesheli kwa watu wenye mahitaji spesheli.