Muungano wa wamiliki wa shule za kibinafsi nchini unataka wakuza mitalaa ya masomo kuangazia upya mtalaa huo na kuufanyia marekebisho.
Wamiliki hao, kupitia kwa katibu wa kitaifa wa muungano huo Mutheu Kasanga, walisema mtalaa wa masomo wa sasa una upungufu mwingi ambao unapaswa kufanyiwa mrekebisho.
Mutheu alisema iwapo mtalaa husika hautafanyiwa marekebisho, viwango vya ubora wa masomo havitaafikiwa kwa mujibu wa ruwaza ya mwaka 2030.
Akihutubia wamiliki wa shule za kibinafsi kutoka North-Rift siu ya Ijumaa, Mutheu alisema mara ya mwisho mtalaa huo kufanyiwa marekebisho ilikuwa ni mwaka 2003/2004.
Kulingana na afisa huyo, ni muda mrefu sana tangu mtalaa huo ufanyiwe marekebisho, ikizingatiwa umuhimu wa mtalaa husika katika sekta ya elimu.
“Mara ya mwisho mtalaa huu kufanyiwa marekebisho ni mwaka wa 2003/2004, kuna haja ya wadau wote kuhusishwa katika marekebisho ya kuboresha mtaala huo,” alisema Mutheu.
Kiongozi huyo alikosoa serikali dhidi ya kubagua wanafunzi kwa misingi ya shule za umma zile za kibinafsi.
"Hakuna mtoto wa binafsi na wa umma, tunataka watoto wote wahudumiwe kwa njia ya usawa bila kujali shule ambako wanasomea au walisomea,” alisema Mutheu.
Wamiliki hao walipuuzilia mbali dhana kwamba wanafunzi ambao husomea katika shule za kibinafsi ni matajiri.
“Fikra kwamba shule za kibinafsi ni za matajiri inapaswa kutupiliwa mbali kwani shule zaidi ya 76 za kibinafsi ambazo ziko katika mtaa wa mabanda wa Kibera ni za matajiri wangapi,” alihoji Mutheu.