Wanachama wa chama cha ODM katika eneo la Likoni kaunti ya Mombasa wamewataka wasisimazi wa chama hicho nchini kuwahakikisha uchaguzi huru na haki pindi watakapokuwa wakichagua wanachama wapya.
Kulingana na mgombea wa chama hicho katika nafasi ya mwenyekiti eneo hilo la Likoni, Hamisi Domoko, kuna baadhi ya watu flani wameanza kutoa vitisho kwa wagombea huku wengine wakipokea ujumbe mfupi wa kushinikizwa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Akizungumza katika eneo la Miami huko Likoni mjini Mombasa siku ya Jumatano katika mkutano wa kuhamasisha umuhimu wa kupiga kura, Domoko amesema kwamba kuna haja ya uchaguzi huo mdogo kuwa wa huru na uwazi ili kuona kwamba kila wananchi anachangia vyema katika uchaguzi huo mdogo.
“Kuna baadhi ya watu flani wameanza kututumia ujumbe mfupi wa vitisho wakisema kwamba tuachane na mambo ya uchaguzi kwani sisi sio wakenya ambao hatustahili kuwania nyadhfa zozote.Sisi tutasimamia nao kuhakikisha kwamba tunatekelezea wananchi wetu maendeleo kwa chama mashinani,” alisema Domoko.
Aidha amewahimiza viongozi wakuu wa chama hicho cha ODM kuzuia kutokea kwa wizi wa kura huku akiwataka wa Wakilishi wa wadi na wabunge kujitenga na kampeni hizo za uchaguzi wa viongozi wa chama cha ODM mashinani.
“Tunataka viongozi wetu wakuu wa chama cha ODM kuwaonya wabunge na wawakilishi wa wadi kujitenga na kampeni hizi kwani huenda wakavuruga uchaguzi wetu wa mashinani,” aliongeza Domoko.
Kura hizo zimepangwa kufanyika tarehe tatu mwezi huu wa Octoba katika kaunti ya Mombasa ili kuwachagua viongozi wengine wa chama cha ODM katika maeneo ya mashinani kabla ya uchunguzi mkuu wa mwaka wa 2017.