Wanachama wa chama cha ODM katika Kaunti ya Mombasa wameeleza wasiwasi wao kutokana na baadhi ya wawakilishi wa wadi kutoka chama hicho kumshtumu Naibu mwenyekiti wa chama hicho.
Wakizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, wanachama hao wakiongozwa na Mwinyi Mwenza walisema kwamba viongozi hao wa kisiasa wameonekana hadharani wakimshtumu naibu mwenyekiti wa chama hicho Hassan Joho kwa madai ya kuongoza chama hicho kwa malengo ya kibinafsi.
Mwenza alipinga madai ya baadhi ya viongozi hao na kusema kwamba Mwenyekiti wa chama hicho Raila Odinga hajawahi lalamika kuhusu utendakazi wa naibu wake huyo,hivyo basi hawana haki ya kumjadili Joho hadharani.
“Tunashangazwa sana na baadhi ya wanachama cha ODM kwa kumshtumu naibu mwenyekiti wa chama hicho Hassan Joho ilhali kiongozi mwenyewe wa chama hajawahi lalamika kuhusu utendakazi wake. Sisi tunasema ikiwa wanamalengo yao basi wajitokeza na waseme badala ya kuonekana hadharani wakitupia cheche za maneno,” alisema Mwanza.
Mchakato huo wa kisiasa umetokana na kikao cha hivi majuzi katika eneo Bunge la Nyali kilichowajumuisha viongozi mbalimbali wa kisiasa.
Viongozi hao walimshtumu Naibu Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho wakitaka ajiuzulu wadhfa huyo la sivyo wataanzisha mchakato wa kura ya maoni kutoka kwa wanachama ili kumbandua katika wadhfa huo.
“Tumechokeshwa na uongozi wa Joho kwa jinsi anavyo ongoza chama. kwa sasa yeye anaegemea upande mmoja pekee na wala hataki kukosolewa kama kiongozi. Hilo sisi hatutalikubali kamwe,” alisema mwakilishi wa Wadi ya Kadzandani Mohammed Ndanda.
Hata hivyo viongozi hao walisema kwamba iwapo Kiongozi wa chama hicho Raila Odinga na wanachama hawatachukua jukumu la dhararu kumchagua naibu mwenyekiti mwingine, basi hawatamuunga mkono wakati wa uchaguzi mkuu ujao.