Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi waliokuwa wamerejea shuleni Jumatatu kulingana na amri ya serikali walilazimika kurudi nyumbani katika shule nyingi za wilaya ya Nakuru Kaskazini baada ya waalimu kukosa kufika.

Wanafunzi wa Kiamaina, Osembo, Kagoto na ile ya St Lwanga walilazimika kurudi nyumbani kwani masomo hayangeendelea bila walimu.

Hata hivyo, baadhi ya waalimu wakuu wanafika shuleni sio kusomesha lakini kuangalia ‘mali ya serikali’ isiharibiwe.

Mmoja wao aliyomba kubana jina alisema, “Mimi na naibu wangu tumekuja kuhakikisha kila kitu kiko shwari, ijapokuwa ni wanafunzi wa darasa la nane pekee ndio wanasoma peke yao. Wengine tumewarudisha nyumbani tukisubiri amri ya wakuu wetu (Knut na Kuppet)."

Mgomo wa waalimu ambao umetokana na mzozo wa nyongeza ya mshahara wao kwa kati ya asilimia 50 hadi 60, umeingia wiki yake ya tano huku serikali ikiendelea kusisitiza kwamba haina fedha za kutekeleza amri hiyo ya mahakama ya kiviwanda iliyotolewa na jaji Nduma Nderi.

Siku ya Ijumaa, serikali ilitangaza shule zingefunguliwa Jumatatu baada ya uamuzi wa korti kuwa waalimu warejee shuleni na serikali kutafuta suluhu ya mzozo huo kwa siku tisini.

Hata hivyo muungano wa waalimu wa Knut ulisisitiza kwamba wanachama wao hawangerudi darasani hadi wakutane na kuelewana.

Mawakili wa serikali na wale wa miungano ya waalimu wanaendelea kusuguana kisheria mahakamani kujaribu kutatua mzozo huo.