Naibu katibu wa chama cha KNUT tawi la Kisii kusini Victor Ombasa amewaomba wanafunzi ambao wana nia ya kusomea ualimu kutopoteza imani na taaluma hiyo kwani watakuwa walimu wa siku sijazo.
Hii ni baada ya idadi kubwa ya wanafunzi katika kaunti ya Kisii kusikika wakisema kuwa hawatasomea taaluma hiyo kufuatia walimu kulipwa mshahara duni na kugoma kila wakati, jambo ambalo limeonekana kuwaogopesha kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii wakati walimu hao wa Knut waliandamana huku wakishirikiana na walimu wa chama cha Kuppet, Ombasa aliwaomba wanafunzi walio na nia ya kusomea ualimu kuisomea kwani kwa sasa maisha mazuri ya walimu yanaendelea kutengenezwa kupitia mgomo unaoendelea.
Aidha, katibu huyo alisema kwa sasa walimu wanaendelea kupitia changamoto nyingi ambazo alidai kuwa huenda zikafika mwisho na kuongezewa mshahara.
Walimu wa vyama hivyo viwili wametishia kufanya jambo mbaya zaidi nchini ambalo hawakulizungumza kwa waandishi wa habari, na kukiri kuwa waandishi wa habari pamoja na wananchi watalishuhudia hivi karibuni ikiwa serikali haitaafikia matakwa yao .
“Rais Kenyatta pesa si zake, ni za mwananchi ambaye hutozwa ushuru. Mbona hataki kuachilia pesa? Pesa za mishahara ni za mwananchi wa kawaida, naomba aheshimu uamuzi wa mahakama na kuachilia pesa,” alisema Ombasa.