Jonuba Bekah, kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Nakuru, amesema kuwa msalaba unaotumiwa na shirika hilo halihusiana kwa vyovyote vile na dini yoyote ile.
Akizungumza kwenye shughuli ya kutoa mafunzo kwa wanahabari wa Nakuru kuhusiana na jinsi shirika hilo linavyofanya kazi yake katika hoteli ya Legacy iliyo Nakuru siku ya Alhamisi, Bekah alisema kuwa msalaba unaotumiwa na shirika hilo ulitokana na bendera ya Uswizi.
Hata hivyo, alisema msalaba ulio kwenye bendera ya Uswizi ambao ni mweupe ulibadilishwa rangi na kufanywa kuwa mwekundu na shirika hilo huku upande wa nje wa bendera hiyo ya Uswizi ambao ni mwekundu ukibadilishwa rangi na kufanywa kuwa mweupe na shirika hilo.
“Msalaba unaotumiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu hauhusiana kwa njia yoyote na dini. Msalaba unaotumiwa na shirika la msalaba mwekundu ulitoka kwa bendera ya Uswizi. Misalaba inayotumia na dini ni mirefu kwa upande wa chini ilhali msalaba unaotumiwa na shirika la msalaba mwekundu unatoshana kwa pande zote,” alisema Bekah.
Kwa upande, mwingine, alisema kuwa Shirika la Msalaba Mwekundu sio shirika lisilokuwa la kiserikali kama wengi wanavyodhania bali ni shirika linalotoa misaada, ambalo hufanya kazi kwa pamoja na serikali.
Alisema kuwa shirika hilo sio shirika lisilokuwa la kiserikali kwani lilibuniwa chini ya sheria za bunge.
“Shirika la Msalaba Mwekundu sio shirika lisilokuwa la kiserikali kwa kuwa lilibuniwa chini ya sheria za bunge. Pamoja na hayo, shirika hili pia halitambuliwi na baraza la mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwani ni lazima mashirika yote yasiyokuwa ya kiserikali yatambuliwe na baraza hili,” alisema Bekah.