Mkuu wa polisi kaunti ya Nyamira Ricah Ongare amewaomba wananchi wote kutochukua sheria mikononi mwao jamb0 mbaya linapotokea ila kuelekea katika kituo cha polisi na kupiga ripoti.
Hii ni baada ya mshukiwa mmoja wa wizi kuteketezwa mnamo siku ya Jumatatu na umati wa watu uliojawa na gadhabu katika soko la Kebirigo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika mji wa Nyamira, Ongare aliomba wananchi kutoteketeza watu ovyo ovyo kwani vituo vya polisi viko na vinastahili kushughulkulia visa kama hivyo.
“Katika nchi yetu ya Kenya, hakuna kipengele hata kimoja katika katiba ambacho kinaruhusu wananchi kuteketeza wenzao haswa jambo mbaya linapotokea, ndio maana vituo vya polisi vikajengwa kila mahala hapa ambapo shida zote hutatuliwa na maafiasa wa polisi,” alihoji Ongare.
Hii si mara ya kwanza wananchi wa kaunti hiyo ya Nyamira kuteketeza watu ambao ni washukiwa wa wizi, lakini kwa sasa wameonywa vikali kutofanya hivyo kwani kuna sheria ambayo inastahili kufuatwa.
“Uchunguzi unafanya katika idara ya polisi wakati ripoti imepigwa na watu husika na sio kufanya maneno kutoka popote pale,” aliongeza Ongare.