Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wananchi katika sehemu ya Chepilat wilayani Borabu walikabiliana vikali na maafisa wa polisi baada ya kuandamana wakilalamikia ukosefu wa matuta barabarani katika sehemu hiyo, hali ambayo imepelekea visa vingi vya ajali kuendelea kushuhudiwa.

Kisa cha hivi karibuni ni cha wiki jana ambapo watu saba waliaga na wengine kuaachiwa majeraha mabaya baada ya lori lililokuwa likiendeshwa kwa kasi mno kukosa mwelekeo na kuwaangukia kando ya barabara katika sehemu hiyo ya Chepilat kwenye barabara kuu ya Keroka -Sotik.

"Tumeendelea kuwapoteza watu wetu kwa visa vingi vya ajali kutokana na madereva ambao huendesha magari kwa kasi kwa sababu ya ukosefu wa matuta ya barabara, na hivyo basi tumeamua kuandamana ili serikali yetu iingilie kati na kutusaidia kabla ya madhara zaidi," mmoja wao alisema.

Hali hiyo iliwabidi magavana John Nyagarama wa kaunti ya Nyamira na wa kaunti ya Bomet Isaac Ruto kuzuru sehemu hiyo na kuwatuliza wananchi, ambapo wote wawili walitoa kila mmoja shilingi laki mbili ili kugharamia matibabu ya walioumia kwenye ajali hiyo na pia mazishi ya walioaga.

Pokea rambirambi zetu kwa huu msiba na mchango huu wa shilingi laki nne utawasaidia waathriwa kwa hivi sasa na tunatarajia kuchanga pesa zaidi za kuwasaidia," walisema Nyagarama na Ruto.

Magavana hao wameitaka serikali kuu kuziwaachia serikali za kaunti mpango wa ujenzi na ukarabati wa barabara ili wawe wakishughulikia kwa kaunti inavyostahili.

Shughuli ya kuwekwa kwa matuta ilianzishwa baada ya viongozi hao miongoni mwa wengine katika sehemu hiyo kutoa msaada wa mchanga, kokoto na simiti ili kufanikisha shughuli hiyo.