Wakenya wameombwa kutowatenga watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi almaarufu zeruzeru ili kuimarisha utangamano nchini.
Akiongea kwenye uga wa Uhuru Gardens mjini Nyamira wakati wa hafla ya kuwahamasisha watu wanaoishi na tatizo hilo la ngozi, mkurugenzi wa mipango kwenye shirika la hamasisho la zeruzeru nchini Timothy Aseka alisema kuwa shirika hilo limekuwa likipokea malalamishi ya kuteswa na kutumiwa vibaya katika jamii, jambo ambalo si zuri.
"Tumekuwa tukipokea malalamishi mengi kuwa baadhi ya watu katika jamii huwatesa watu wanaoishi na ulemavu huo, jambo ambalo sio zuri," lisema Aseka.
Afisa huyo aliongeza kusema kuwa serikali inafahamu fika changamoto wanazokumbuna nazo zeruzeru hao, akisema kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa maslahi ya watu hao yanashughulikiwa kwa kuwapa mafuta spesheli ya kujipaka ili kuzuia ngozi zao kuchipuka na kadhalika.
"Serikali inafahamu fika matatizo wanayokumbana nayo walemavu wa ngozi na huwasaidia na mafuta yakujipaka ili kuzuia ngozi zao kuchipuka, kuwapa matibabu ya bila malipo kwenye hospitali za umma, kuwapa kofia zakujikinga na miale mikali ya jua na maslahi mengine," aliongezea Aseka.