Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa maswala ya watoto katika kaunti ya Nakuru, Abdi Yusuf ameonya kwamba wale wanaoendesha makao ya watoto pasi na kusajiliwa chuma chao kimotoni.

Akizungumza na wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne, Yusuf alisema watafanya msako wa kutathmini ni makao yepi ya watoto ambayo yanahudumu kinyume cha sheria.

Yusuf alielezea wasiwasi wake kwamba kuna baadhi ya watu wanaoendesha makao ya watoto wakiwa na lengo la kupata pesa kutoka kwa wafadhili, huku watoto walengwa wakikosa kunufaika na misaada hiyo.

“Baadhi ya vitu ambavyo tutakuwa tukiangalia ni vyeti rasmi vya kuhudumu kwa makao hayo, hali ya mazingira ya makao hayo miongoni mwa mambo mengine,” alisema Yusuf.

Ijapokuwa hakuelezea ni lini watafanya operesheni hiyo, Yusuf alisisitiza kuwa operesheni hiyo ni muhimu kwani itawawezesha kuwakamata na kuwafunguliwa mashtaka wenye makao hayo, kwa kutumia watoto kama kitega uchumi.

Hata hivyo, Yusuf ametoa wito kwa umma kuwa macho na kuripoti visa vyovyote vya unyanyasaji wa watoto wanaoishi katika makao ya watoto pamoja na maeneo mengine ili watuhumiwa wafunguliwe mashtaka.