Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamishna mpya wa Kaunti ya Nakuru Joshua Nkanatha, amesema kuwa wanaotumia leseni zao kuuza vileo haramu watajipata taabani.

Akizungumza katika hafla ya maombi ya kwanza ya kaunti yaliyofanyika wakati wa kiamsha kinywa siku ya Ijumaa katika uwanja wa mkahawa wa Rift Valley Sports Club Nakuru, Nkanatha alisema kwamba yeyote anayetumia leseni hiyo vibaya atakamatwa na kushtakiwa, huku yule aliyetoa leseni hiyo akichukuliwa hatua sawia.

“Ikiwa unatumia leseni kuuza vileo haramu kisha unavificha tunapofanya msako, tutakukamata na yule ambaye alikupa leseni hiyo pia atakamatwa,” alisema Nkanatha.

Aidha, alisema kwamba hatavumilia afisa yeyote aliye chini yake ambaye hatakabiliana na pombe hiyo haramu akisema kwamba endapo afisa huyo atagunduliwa, atapigwa kalamu mara moja.

Kulingana naye, msako dhidi ya pombe haramu kwenye Kaunti ya Nakuru utazidi kuendelezwa ikizingatiwa kuwa uuzaji na utengenezaji wa pombe haramu umeanza kurejea tena.

Wakati huo huo, amewataka wadau wote kufanya kazi kwa pamoja naye ili kumaliza pombe hiyo haramu.

“Sitamvumilia afisa yeyote ambaye hafanyi kazi yake ya kukabiliana na pombe haramu kikamilifu. Nitakapogundua hilo, afisa huyo atakwenda nyumbani kwani siwezi fanya kazi na mtu kama huyo,” alisema Nkanatha.

Kamishna huyo aliahidi kutumikia kaunti ya Nakuru kikamilifu pamoja na taifa la Kenya kwa jumla.

“Ni lazima tutumikie kaunti hii na taifa hili kwa ujumla kwa njia ifaayo,” alidokeza Nkanatha.

Nkanatha alichukua nafasi yake Mohammed Birik ambaye alikuwa kaunti kamishna wa Nakuru.