Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amewataka vijana waliyojitosa katika utumizi wa mihadarati kujiwasilisha kwa viongozi pamoja na maafisa wa usalama, la sivyo atawashinikiza maafisa wa usalama kuwatia nguvuni.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Abdulswamad alisema kwamba iwapo vijana hao watajitolea kikamilifu na kujiwasilisha kwa viongozi na maafisa wa usalama, basi visa vya kihalifu vitapungua kwa kiasi kikubwa katika kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Abdulswamad, idadi kuwa ya vijana waliyojiunga na mihadarati hukiri kujiwasilisha, kisha baadaye hutoroka katika vituo vya kurekebisha tabia wakidai kukosa hudumu bora kutoka kwa wanaohusika na tiba maalum.

“Idadi kuwa ya vijana hukiri kujinasua katika janga hilo na kupelekwa katika vituo cha kurekebisha tabia, na baada ya muda huvitoroka vituo vile. Kama viongozi, hilo hatukubaliana nalo lazima vijana wajitolee kupata matibabu ili tuweze kupunguza kukithiri kwa visa vya uhalifu,” alisema Abdulswamad.

Abdulswamad amewataka vijana hao kurejea mara moja katika vituo hivyo vya kurekebisha tabia waraibu wa mihadarati ili kuona kwamba swala la utumizi wa mihadarati linasitsishwa katika kaunti hiyo ya Mombasa.

Aidha, ameahidi kuwashinikisha maafisa wa usalama kuwakabili vijana hao iwapo watakaidi kujiwasilisha kwani hatua hiyo inazidi kurudisha nyuma juhudi za viongozi na wanaharakati wa maswala ya kijamii katika kupiga vita mihadarati kaunti ya Mombasa na eneo zima la pwani.

Hata hivyo, zaidi ya vijana 100 wanakisiwa kutoroka katika vituo hivyo vya kurekebisha tabia waraibu wa mihadarati baada ya vijana hao kudai kupitia hali ngumu ya maisha pamoja na kukosa hudumu bora.