Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa kisiasa kutoka Masaba, Kaunti ya Kisii, wameikosoa hatua ya serikali kufunga shule nchini huku wakisema kuwa visa vya mimba za mapema na ulevi vitaongezeka miongoni mwa vijana.

Wakiongea siku ya Jumapili katika hafla ya kutafuta njia mbadala ya kumaliza mgomo wa walimu katika hoteli moja mjini Kisii, viongozi hao walisema watashinikiza serikali kuzifungua shule haraka iwezekanavyo ili kueneza usawa wa masomo nchini kwani shule za kibinafsi zingali zinaendelea na masomo yao ya kawaida.

Viongozi hao wakiongozwa na Benard Moseti, wameitaka serikali kufanya mazungumzo na vyama vya walimu ilikupata suluhu la mgomo huo wa walimu.

“Sisi kama viongozi wa kisiasa kutoka Masaba kusini tunataka shule zifunguliwe mara moja maana kuwepo kwa watoto nyumbani na karo tayari imelipwa itakua njia moja ya kuregesha maendeleo ya taifa nyuma. Serikali na walimu wakae waongee ili waafikiane watoto wetu warudi shuleni,” alisema Moseti.

Aidha, wawakilishi wadi tofauti kutoka eneo hilo pia walikashifu serikali kwa kusema maisha yamekua magumu mno na basi yapaswa walimu kupewa nyongeza ya mishahara japo sio kiwango na asilimia wanayodai kwa sasa.

“Kama viongozi wa kaunti, tunaitaka serikali kuu kuongea na walimu na kupata suluhu ili wanafunzi miongoni mwa jamii isiyoweza kuwaelimisha wanao katika shule ya kibinafsi pia wapate elimu,” alisema Sammy Keronche, mwakilishi wa wadi ya Gesusu.

Francis Aburi, mwakilishi wa wadi ya Ichuni, alisema kuwa kuna njaa katika eneo hilo na wanafunzi wakirejea nyumbani kutakuwa na shida.

Joash Orora, mwakilishi wa wadi ya Masimba, aliwaomba walimu kuwa watulivu na waketi katika mahojiana na serikali ili kutafuta suluhu.