Mahakama ya Nakuru iliwahukumu wanaumme watano kifungo cha kifo baada ya kuwapata na hatia ya kumuuwa mama moja mkongwe.
Watano hao, Anthony Macharia, Simon Njuguna, John Karia, John Nganga na Peter Matheri walipatikana na kosa la kumshambulia na kusababisha kifo cha mkongwe huyo kwa jina la Ann Wanjiku mnamo tarehe Juni 5, mwaka wa 2010 katika kijiji cha Kisumu Ndogo eneo la Kipipiri, katika kaunti ya Nyandarua.
Akitoa ushahidi mahakamani, Damaris Muthoni ambaye ni dadake marehemu, alijuza mahakama kwamba walikuwa nyumbani wakati ambapo washtakiwa waliingia na kuanza kumshambulia dada yake huku wakimburura.
Kwa muujibu wake, juhudi zake za kuingilia kati ziliambulia patupu kwani pia yeye aliadhibiwa vikali.
Shahidi mwingine ambaye ni mpwa wa marehemu kwa jina la Grace Nyambura, naye alijuza mahakama kuwa baada ya marehemu kushambuliwa, alimpeleka hospitalini ambapo aliaga na kulingana naye, marehemu alikuwa majeraha kwenye uso na kichwa.
Washtakiwa hao hata hivyo walijitetea kuwa walikuwa wakiendela na kazi yao siku ya tukio hilo wakiongeza kuwa mashahidi waliwaona walipomchukua marehemu kutoka nyumbani kwake.
Akitoa hukumu yake, Jaji Maureen Odero alisema kuwa ushahidi uliotolewa na baadhi ya mashahidi kuwa marehemu alikuwa akishukiwa kuwaa na vifaa vya uchawi shambani mwake haukuwa sababu tosha ya kumpelekea marehemu kushambuliwa.
Aidha, aliongeza kwamba upande wa mashtaka ulifanikiwa kutoa ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa washtakiwa walimshambulia marehemu na kusababisha kifo chake.
Pamoja na hayo, jaji huyo alikariri kuwa hakuna ushahidi uliodhibitisha kwamba marehemu alikuwa akijihusisha na uchawi, sababu kuu ambayo ilitajwa kama iliyopelekea washthakiwa hao kumshambulia.
Kulingana naye, marehemu angepelekwa kwenye kituo cha polisi badala ya washtakiwa kuchukua sheria mikononi mwao na kumshambulia marehemu.
Washtakiwa hao hata hivyo wana wiki mbili za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.