Share news tips with us here at Hivisasa

Wanawake kutoka Kaunti ya Nyamira wametangaza uwezekano wa kumuunga mkono mmoja wao ili kuwania nyadhifa za juu katika serikali ya Kaunti ya Nyamira.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na wanawake wenye taaluma mbalimbali katika mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa kamati hiyo Bi Susan Onyamo, alisema kwamba kuna uwezekano wa kumteua mmoja wao kuwania ugavana ama kungangania cheo cha spika kwenye bunge la kaunti hiyo.

"Wanawake wapiga kura katika kaunti hii ni wengi na hatuoni sababu yakutomuunga mkono mmoja wetu kuwania vyeo vitatu vikiwemo ugavana, unaibu wa ugavana na pia kiti cha spika wa bunge la kaunti. Tutafanya maamuzi hayo mwisho wa mwezi Disemba ili kumuidhinisha mmoja wetu,” alisema Onyamo.

Wanawake hao aidha waliongeza kwa kusema kuwa hatua hiyo itawapa motisha wanawake wengine kujitokeza kuwania nyadhifa za uwakilishi wa maeneo wadi kwenye bunge la kaunti hiyo.

"Nia yetu sio tu kumteua mmoja wetu kuwania nyadhifa kuu kwenye serikali ya kaunti bali pia ni kuwapa hamasa wanawake wengine kujitokeza na kuwania nyadhifa za uwakilishi wa maeneo wadi ile iwe rahisi kupigania haki zetu,” alisema Onyamo.

Bunge la kaunti ya Nyamira lina wawikilishi wadi wanawake wawili pekee waliochaguliwa akiwemo mwakilishi wa wadi ya Esise Theresa Nyaanga, na mwenzake wa Bokeira Karen Atuya.