Wanawake katika kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujitokeza na kujiunga na makundi ya kimaendeleo ili kunufaika na miradi mbalimbali inayotolewa na serikali kuu.
Akiwahutubia makundi ya wanawake mjini Mombasa siku ya Jumanne, Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake kaunti ya Mombasa Afiya Rama alisema kwamba serikali imejitolea kuwasaidia akina mama kufanikisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kujikimu kimaisha.
Kulingana na Rama, wanawake wengi katika kaunti ya Mombasa wamesalia nyuma kimaendeleo kutokana na kukosa mwongozo mwafaka wa kufanikisha malengo yao mashinani, huku akisema kwamba kupitia hamasa katika vikundi vya akina mama basi jamii itapiga vita umaskini.
“Tungewaomba wanawake mjitokeze na kujiunga na makundi ya wanawake ya maendeleo ili nanyi pia muweze kufaidika na miradi inayotolewa na serikali kuu. Ni lazima kubuni vikundi vitakavyowawezesha kupata miradi ile,” alisema Rama.
Alisema kwamba maafisa wa chama hicho wamezuru mashinani kuvielimisha vikundi vya akina mama na vijana jinsi ya kutumbua umuhimu wa kujiunga na makundi ya kimaendeleo pamoja na kunufaika na miradi mbalimbali inayotolewa na serikali.
“Tayari tumetuma maafisa wa chama chetu cha maendeleo ya wanawake kuzuru mashinani na kuwaelimisha wanawake kufahamu mengi katika kujiunga na makundi ya wanawake ili waweze kujikimu na miradi na mikopo itayaotolewa kutekeleza miradi,” aliongeza Rama.
Mwenyekiti huyo wa chama cha maendeleo ya wanawake ameahidi kuwaunganisha akina mama mashinani na kuwaeleimisha jinsi ya kujihusisha na biashara ndogo ndogo zitakazowawezesha kupata pato bora la kuwakimu kimaisha mashinani.