Daktari Weston Khisa amewahimiza wanawake wajawazito kutembelea hospitali kabla ya kujifungua ili kunufaika na huduma tofauti haswa kupimwa magonjwa mbalimbali.
Wito huo umetolewa baada ya uchunguzi kufanywa na kubaini kuwa baadhi ya wanawake waja wazito hawatembelei hospitali hadi siku ya kujifungua kufika na wengine kujifungulia nyumbani.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii, Dkt Khisa alisema wengi wa wanawake ambao hujifungulia nyumbani huathirika na ugonjwa wa fistula kufuatia kutojua taratibu za kufuata wakati wa kujifungua.
Daktari huyo aliwaomba wanawake wajawazito kutembelea hospitali kila wakati ili kuzuia changamoto ambazo huwakumba wakati wa kujifungua kama vile ugonjwa wa fistula na magonjwa mengine ambayo yanaweza athiri afya yao.
“Baadhi ya akina mama hawatembelei hospitali ili kupimwa. Wengi hawaendi hospitali kujua hali zao na kupewa maelezo jinsi ya kujitunza wakiwa na mimba kabla ya kujifungua jambo ambalo huleta shida kwa akina mama wengi huku wengi wakiathirika na ugonjwa wa fistula,” alisema Dkt Kisha.
Daktari huyo alisema baadhi ya visa vya akina mama kujifungua kabla ya miezi tisa kukamilika husababishwa na kutofuatilia maelezo wanayopewa kutoka kwa kliniki za ujauzito.
“Wanawake hawatakuwa na changamoto kama za kuathirika na ugonjwa wa fistula, kujifungua mapema ikiwa watafuata ushauri wa kuenda kliniki na kufuata maelezo kamili watakayopewa,” aliongezea Khisa.
Hospitali hiyo imefungua kambi ya kutoa matibabu ya bure kwa wagonjwa wanaougua ugonjwa wa fistula.