Wanabodaboda wawili na abiria watatu walinusurika kifo baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabara baada ya kugongwa na matatu aina ya Nissan katika barabara kuu ya Ram, kutoka mjini Kisii kuelekea Keroka siku ya Jumatano mchana.
Kulingana na mshirikishi mkuu wa wenye bodaboda katika kaunti ya Kisii ambaye alishuhudia ajali hiyo Joseph Mogambi, watu hao waligongwa na matatu hiyo ya abiria walipokuwa wakitoka steji wakielekea njia ya Daraja Moja, wakati ambapo gari hilo ambalo lilikuwa linatoka nyuma yao lilipoteza mwelekeo na kuwagonga na kuwajeruhi vibaya.
Mogambi aliongeza kusema kuwa mwanabodaboda mmoja ambaye alikuwa amembeba mama mjazito walijeruhiwa vibaya katika kisa hicho .
“Gari hiyo aina ya Nissan ilipoteza mwelekeo na kuwagonga wenye pikipiki wawili na abiria wao na kuwarusha kando ya barabara, na dereva wa gari hilo ndiye alikuwa anaendesha gari lake vibaya kwa vile sehemu hii ina mashimo mengi,” alisema Mogambi.
Hata hivyo, alisema kuwa dereva wa matatu hiyo aliweza kutoka na kutoroka na kuiacha matatu hiyo mahali pa ajali kwa kugopea kupigwa na watu pamoja na vijana wa pikipiki ambao walikuwa na hasira.
Kiongozi huyo wa bodaboda alitoa wito kwa wenye magari na watumizi wa barabara kwa jumla kuwa waangalifu wanapokuwa wakiendesha mitambo yao.
Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali kuu ya Kisii Level Six kwa matibabu, huku gari hilo pamoja na pikipiki hizo mbili zikipelekwa katika kituo cha polisi cha Kisii Central.