Watu wanne walifikisha katika mahakama moja mjini Eldoret siku ya Jumanne na kushtakiwa kwa kosa la kuuza pombe haramu.
Godfrey Agali, Salome Waithera, Rosemary Naliaka na Martine Wanjala, walishtakiwa kwa kosa la kutengeneza na kuuza pombe haramu katika eneo la Langas.
Washukiwa hao walikamatwa na pombe haramu kwa ushirikiano wa Polisi na askari wa Kaunti ya Uasin Gishu siku ya Jumatatu.
Mahakama ilielezewa kwamba, wanne hao walinaswa baada ya askari wa kaunti kupata habari kutoka kwa wakazi kuwa wanaendeleza biashara hiyo isiyo halali.
Godfrey alishikwa na zaidi ya lita 65 ya changaa, Salome alishikwa na zaidi ya lita 20 ya changaa na lita 20 ya kangara, Rosemary alishikwa na lita 10 ya changaa na 40 ya kangara ilhali Martine alishikwa na lita 20 ya kangara.
Wanne hao walikubali mashtaka hayo na kumuomba Hakimu Mkuu Margaret Wambani kuwaachilia kwa dhamana kwani walikuwa na watoto wadogo nyumbani.
Godfrey Agali alipewa faini ya Sh50,000 Salome Sh35,000, Rosemary Sh30,000 na Martine Sh 25,000.
Aidha, Joseph Koech na Joshua Mutiti walishtakiwa katika mahakama hiyohiyo kwa kosa la kuwa walevi kupindukia na kutoa maneno ya matusi kwa watu.
Hakimu alimuamuru wawili hao walipe faini ya Sh500 kila mmoja au kifungo cha wiki moja gerezani.