Wapigambizi wameitaka serikali za Kaunti ya Mombasa kuwapa ajira ili kuwasaidia wageni ambao huzuru fuo mbali mbali za bahari Hindi.
Vijana hao walisema kuwa vifo ambavyo vilitokea hivi karibuni kama vile vya wanafunzi kutoka eneo la kati la Kenya kuzama havingetokea iwapo wapigambizi wangekuwa katika maeneo hayo, ili kuwaongoza na kuwaelekeza wageni ambao wengi hutoka bara na hawana ujuzi wa kuogelea baharini.
Akiongea kwa niaba ya vijana hao siku ya Jumapili katika ufuo ya Mama Ngina mjini Mombasa, msimamizi wa kikundi cha Pwani-10-Divers, Borniface Ngala, alisema kuwa kwa muda mrefu sasa fuo za bahari Hindi hazijakuwa na wataalamu wa kupigambizi ambao wameajiriwa mbali na wale wa kikosi cha wanajeshi wa maji ambao mara nyingi hujihusisha na shughuli hiyo wakati kumeripotiwa janga la watu kufa maji.
“Hali hii sharti iangaliwe na tunaomba serikali ya kaunti iwape vijana kazi ya kuhudumu kwenye fuo hizo,” alisema Ngala.
Aidha, alimwomba Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, kuwatambua vijana hao ambao huwatembeza watalii fuoni kwa kuwapa hati maalumu za kuwatambua kwenye shughuli zao.
Ngala alisema kuwa shughuli ya kuokoa maisha ya wale ambao hawana ujuzi wa kuogolea ni ya muhimu mno kwao kwa vile ndio inawalisha wengi wao.
Aliongezea kuwa huwa vigumu wageni kuwatambua wanapojaribu kuwaongoza kwa vile wageni hao mara nyingi hukataa kuwalipa na kuwataka kutoa vitambulisho vya kuwahalalisha kufanya shughuli hiyo.