Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maafisa wa polisi katika Kaunti ya Nyamira wamewatia mbaroni washukiwa sita wa wizi wa magari katika Wilaya ya Ting’a.

Akizungumza na Waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, mkuu wa wa idara ya uchungunzi, Kaunti ya Nyamira George Nyaga alisema waliwatia mbaroni washukiwa hao siku ya Jumatatu.

Alisema washukiwa hao tayari walshaiba gari aina ya Nissan kutoka mji huo wa Nyamira siku ya Jumamosi usiku na kulipeleka hadi eneo lingine la Rongo katika Kaunti ya Migori.

Afisa huyo alisema washukiwa hao walikuwa tayari wamebadilisha rangi ya gari hilo na hata kulibadilisha nambari ya usajili wa gari hilo.

Maafisa hao wa polisi waliwafuata hadi eneo hilo la Rongo na kuwatia mbaroni sita hao baada ya kupokezwa habari kutoka kwa wakazi.

Wizi wa aina hiyo umekuwa ukishuhudiwa sana kila wakati katika Kaunti ya Nyamira, jambo ambalo limewapelekea wakazi wa eneo hilo kuhofia usalama wao.

Uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na wizi huo na washukiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumanne kujibu mashtaka hayo ya wizi.

"Watu walio na tabia ya wizi wa aina yoyote siku zao zinaendelea kuhesabiwa na hawatakuwa na nafasi katika jamii," alihoji afisa Nyaga.