Hali ya kizaazaa na huzuni ilizuka katika hospitali ya Kangundo Level Four siku ya Alhamisi, baada ya watoto sita kupoteza maisha yao kutokana na sababu tofauti baada ya wazazi wao kujifungua vizuri. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizunguza na kundi la wanahabari ofisini mwake, msimamizi wa matibabu katika hospitali hiyo alisema kuwa watoto hao waliaga kutokana na kuzaliwa kabla ya wakati wao kufika, na pia kuzaliwa kabla kufikisha kilo mbili nukta tano.

"Kuna uwezekano mkubwa mtoto akafa iwapo amezaliwa kabla ya wakati wake au kuzaliwa akiwa chini ya kilo mbili, na hivyo hicho ndicho kilifanyika," alisema afisa huyo.

Wazazi wa watoto hao walilaumu usimamizi wa hospitali ile na kusema kuwa vifo vya watoto wale vingezuiliwa iwapo hatua za dharura zingechukuliwa. 

Mzazi mmoja alisema kuwa utepetevu wa hospitali hiyo ya iliyo katika kaunti ya Machakos ndio ulisababisha vifo vile, na kumwomba waziri wa afya katika serikali kuu James Macharia kuchunguza matibabu katika hospitali hiyo kujua kiini hasa cha vifo hivyo. 

"Nmempoteza mwanangu na inauma sana kwani nlimtazama mwanangu akidungwa sindano tano akitafutwa mshipa jambo lililonikera kabla ya saa chache kupata habari mwanangu ameaga dunia," alisema mzazi huyo aliyekataa kutajwa jina.

"Ningeomba uchunguzi wa dharura uanzishwe katika hospitali hii ili kubaini nini hasa kilisababisha vifo hivi ili kuzuia watoto wengine kupoteza maisha yao," aliongezea mzazi huyo.