Share news tips with us here at Hivisasa

Watu saba wamethibitishwa kuaga dunia kwenye ajali mbaya iliyofanyika katika barabara ya kutoka Sotik kuelekea Chepilat katika barabara kuu ya Keroka-Kericho, katika wilaya ya Borabu kwenye kaunti ya Nyamira siku ya Ijumaa jioni.

Akithibisha ajali hiyo, mkuu wa polisi katika eneo hilo la Borabu Jonathan Ngala alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari moja ambalo lilikuwa limebeba kuni na lilikuwa katika barabara kuu ya Sotik-Chebilat, ambapo liligongana na gari aina ya Matatu ambayo ilikuwa inatoka kwenye upande mwingine.

Afisa huyo alisema kuwa lori hilo liliweza kugonga watu wengine ambao walikuwa kando ya barabara, na kuwaua watatu miongoni mwao na wengine wanne kutoka kwenye matatu hiyo ambayo ilikuwa njiani kuelekea Sotik.

Kulingana na mmoja wa wakazi ambaye alishuhudia ajali hiyo, Samson Nyariki, gari hilo la Kuni lilikuwa linaendeshwa kwa kasi, ambapo lilianza kuyumbayumba na likakutana na gari hiyo aina ya Nissan ambayo ilikuwa inatoka Keroka.

Afisa huyo wa polisi aliwataka waendeshaji magari kuwa makini hasa nyakati hizi za mvua nyingi ambayo inaendelea kunyesha katika maeneo ya nyanda za juu za Kenya.

Waliojeruhiwa walipelekwa katika kituo cha Gucha mjini Keroka na waliopoteza maisha yao wakapelekwa katika hospitali moja mjini Keroka.