Waumini wametakiwa kuwa macho na kujiepusha na wahubiri bandia pamoja na manabii wanaotumia jina la Mungu kwa manufaa ya nafsi.
Akiongea siku ya Jumamosi katika kanisa la Kisii Central SDA, mhubiri maarufu kutoka nchi ya Malawi Pst Jefferson Mnyenyembe, aliwashauri wakazi pamoja na waumini kutumia muda wao vizuri kwa kusoma bibilia kikamilifu ili kujiepusha kupotoshwa na manabii laghai.
Mnyenyembe alishangazwa ni vile watu wa kizazi cha sasa wamekuwa wakitumiwa kama chambo cha samaki na kuwa mawakala wa kusambaza nguvu za shetani jambo ambalo alisema ni hatari na kusema kuwa waumini wasipokuwa makini watakuja kuangamizwa na mienendo mibaya.
Huku akinukuu vifungu mbali mbali kutoka katika Bibilia, aliwasia na kuwashauri waumini kuwa watu wa kuomba sana kwani Mungu hakosi kusikiliza maombi ya waja wake.
Aidha, aliwashukuru waumini wa kanisa hilo kwa kuwa na unyenyekevu na kuwataka waliohudhuria sala hiyo, kuwa mabalozi wema kwa kusambaza ujumbe kwa rafiki zao.
“Ningependa kuwaomba waumini kuwamakinisha waumini wenzao na wale walio na azma ya kubadilisha nyoyo zao dhidi ya unabii na manabii bandia,” alisema Mnyenyembe.