Wawakilishi wa wadi katika Kaunti ya Kisii wameomba wanakandarasi katika kaunti hiyo kuchunguzwa kabla ya kupokezwa kandarasi zozote ili kuzuia uharibifu wa pesa za serikali.
Wito huo umetolewa baada ya mwanakandarasi aliyepokezwa kandarasi ya kuweka na kukarabati chemichemi za maji katika Wadi ya Moticho iliyoko eneo bunge la Mugirango kusini, kufanya kazi hiyo vibaya na kuagizwa kuirudia.
Ombi hilo lilifikishwa mbele ya wawakilishi hao na mwakilishi wa wadi ya Moticho, Evans Mokoro, aliyelalamikia kazi hiyo mbaya, jambo ambalo liliwalazimu wawakilishi kupitisha mswada kuwa wanakandarasi wanapswa kuchunguzwa kwanza kabla ya kukabidhiwa kazi.
Wawakilishi hao chini ya uongozi wa spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki, walichagua kamati rasmi ya kufanya uchunguzi huo wa wanakandarasi siku ya Alhamisi.
Kamati hiyo itakayo ongozwa na mwenyekiti Charles Nyagoto itakuwa ikitekeleza shughuli ya kuchunguza wanakandarasi kabla ya kupewa kandarasi kwani imebainika kuwa wengi wao hufanya kazi vibaya na pesa za mwananchi hupotea kwa njia isiyo halali.
Chemichemi hizo tano ambazo hazikutengenezwa kwa kiwango ni chemichemi ya Getongo, Nyasembe, Nyatenga, Riabunduki na Riogeto.
Kila chemichimi ilitengewa Sh200,000 pesa ambazo wawakilishi walisema ni nyingi, na kutaka chemichemi hizo kutengenezwa kulingana na kiwango cha pesa.
Mwanakandarasi huyo alipigwa marufuku na wawakilishi wa wadi waliosema hatafanya kazi tena katika kaunti hiyo.