Wawakilishi wadi mbali mbali kutoka eneo bunge la Nyaribari Masaba wameahidi kushirikiana na mbunge wa eneo hilo kimaendeleo ili kuafikia malengo ya ruwaza ya 2030.
Aidha, wamesema kuwa eneo hilo linalowakilishwa bungeni na Elijah Moindi lajikokota kimaendeleo kwa kile wamedai ni kutotengamana na wakazi wa eneo hilo.
Wakiongozwa na mwakilishi wa wadi ya Nyamasibi, Samson Nyagaka, wawakilishi wadi hao wamemtaka mbunge wa eneo hilo kuwajibika na kutekeleza baadhi ya miradi aliyokua ameanzisha aliye kuwa mbunge wa eneo hilo na sasa balazi wa Kenya profesa Sam Ongeri
Wakiongea siku ya Jumatano katika Soko la Masimba kwenye hafla ya kupanga mradi wa kuinua eneo hilo kimaendeleo, walisema kuwa wanalenga kumsukuma mbunge wa eneo hilo kuwafanyia wakazi kazi.
Joash Orora wa wadi ya Masimba, aliwataka wakazi hao kuwa watulivu na kuwapa wawakilishi hao nafasi ya kuweka kikao na mbunge wao ili kujadili namna na kuleta maendeleo na kumaliza miradi katika eneo hilo.
Mwakilishi wa wadi ya Ichuni Francis Aburi alisema kuwa viongozi wanapswa kuwajibika na kuwafanyia wakazi kazi walioajiriwa kutekeleza.
Sammy Keronche wa wadi ya Gesusu amewataka wakazi wa eneo hilo kuwaheshimu viongozi ili kuwapa wakati wa kuwafanyia kazi.
“Wakazi wa eneo hili wanapaswa kusaidai viongozi katika kutekeleza maendeleo wala sio kujihusisha na siasa za upinzani kila kuchao,” alisema Keronche.