Wanaume wawili kutoka eneo la Gilgil katika Jimbo la Nakuru wameripotiwa kufariki kutokana na ukosefu wa pombe.
Akitoa habari hio jana katika ofisi yake, Kamshina wa Polisi wa eneo hilo bwana Kamau Karungo alithibitisha kwamba mmoja wawili hao aliaga dunia siku ya Jumapili katika kijiji cha Ngomongo baada ya kukosa pombe kwa takriban siku tano huku mwenzake akiaga siku ya Jumamosi. Hii ni kufuatia msako dhidi ya pombe haramu ulioanzishwa hivi majusi.
Akitoa habari hiyo, Kamishna Karungo alisema Maafisa wa serikali katika eneo la Gilgil tayari wameanzisha mpango wa kuwanakili wanaopitia shida ya kimwili kufuatia ukosefu wa pombe mwilini mwao ili kuzuia maafa zaidi.
“Tumeanzisha mpango ambapo tutaweka sajili ya watu wote walioathirika na ukosefu wa pombe katika mwili yao kuhakikisha maafa kama haya hayatokei tena katika eneo hili,” alisema Kamishna Karungo.
Kamishna huyo aliongeza pia kuwa kufikia siku ya kwanza ya shugli hiyo walikuwa wameshasajili watu 30 tayari kuwapa huduma ya kurekebisha tabia ili waweze kuishi bila kutegemea pombe hiyo haramu.
“Tumepokea habari kwamba watu wawili wameshaaga dunia katika kijiji cha Ngomongo na ndiposa tumeanzisha mpango huu wa kuwasajili wote walioathirika ili kuwarekebisha maanake hatutaki vifo zaidi kutokea,” alisema Kamishna Karungo.
Aliongezea kwamba shugli hiyo ya msako dhidi ya pombe haramu imefanikiwa mno katika kupunguza uuzaji wa pombe haramu katika eneo hilo akiongeza kuwa wamefanikiwa kukamata na kuharibu maelfu ya lita za pombe.