Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nyamira Alice Chae amewashauri wazazi kutoka kaunti za Nyamira na Kisii kutowakeketa wanao kwani wao hukumbwa na changamoto nyingi wakati wa kujifungua.
Kulingana na mwaklishi huyo, viwango vya ukeketaji katika kaunti hizo mbili vimepanda licha ya tendo hilo kupigwa marufuku.
Akizungumza na waandishi wa habari Siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, Chae aliwaomba washikadau kujiunga pamoja na kutafuta hatua watakayowachukulia wazazi wanaohusika na ukeketaji.
Chae alisema kuwa ni kinyume na sheria kujihusisha na ukeketaji lakini bado sheria hiyo haijapokelewa vizuri katika kaunti hizo.
“Nashangaa ni kwanini wazazi mumekatazwa kukeketa wasichana lakini bado munaendeleza mila hiyo. Ninaomba washikadau katika eneo la Kisii na Nyamira tuungane pamoja tutafute jinsi ya kutatua shida hii,” alisema Chae.