Wakaazi Mombasa wamepongeza juhudi za mahakama za kuwataka walimu kurudi kazini na kuendeleza shughuli za masomo ambazo kwa muda wa mwezi mmoja zililemazwa.
Siku ya Jumapili, baadhi ya wakaazi hao walitoa shinikizo kwa wanafunzi kutia juhudi katika masomo hata baada ya kukosa usaidizi wa walimu kwa kipindi cha wiki tano, ikizingatiwa kwamba mitihani ya kitaifa imewadia.
Wakaazi hao pia walikashifu uamuzi wa mahakama kwa kutoa maagizo mara mbili hatua iliyowatatanisha walimu kwani licha ya kudai nyongeza yao, walimu hawajalipwa.
“Tumepongeza juhudi za mahakama kuingilia kati mgomo wa walimu na kuusitisha lakini maamuzi yaliyotolewa na mahakama mara mbili ndio yaliyochanganya kusitishwa kwa mgomo huo. Hata baada ya walimu kusitisha mgomo wao bado hawajalipwa nyongeza yao,” alisema mmoja wa wazazi hao.
Aidha wakaazi hao wametoa pendekezo kwa serikali kuongeza mtaala wa masomo ya muhula wa tatu ili wanafunzi waweze kukamilisha masomo yao kwani muda mwingi waliupoteza wakati wa mgomo wa walimu.
“Tungeomba serikali iongeza mtaala wa masomo ya muhula wa tatu kwa wanafunzi kili waweze kukamilisha masomo yao kwani bila ya hatua hiyo kuchukuliwa basi watoto wetu watasalia nyuma kimasomo kila uchao,” alisema mzazi wa watoto wawili.
Walimu wanadai nyongeza ya asilimia 50 hadi 60.