Mwakilishi wa wadi ya Sensi, eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini Ochong’a Nyagaka amewaomba wazazi wote kuwaelimisha watoto ili waweze kujisaidia nyakati zijazo.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa afisini mwake iliyoko mjini Kisii, mwakilishi huyo alisema watoto wakielimishwa, visa vya wizi havitashuhudiwa katika kaunti hiyo.
Aliwaomba wazazi wote wa kaunti ya kisii kuwapeleka watoto wao shuleni ili nao waje kufurahia matunda ya masomo siku zijazo.
“Sioni sababu ya wazazi kutowapeleka watoto wao shuleni kwasababu elimu ni bure. Naomba kila mzazi ampeleke mtoto wake shuleni ili aweze kupata masomo ambayo yatasaidia mtoto maishani,” alisema Nyagaka.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo aliomba walimu kutia motisha kwa kuwasomesha watoto ili waweze kupita katika mitihani ya kitaifa.
Nyagaka alisema ameweka mikakati ya kuwachimbia wakazi wa eneo hilo visima vya maji kando na vile ambavyo amechimba kwa sasa ili wakazi wa wadi yake waweze kunufaika na mradi wa maji.
“Nitajaribu nichimbe visima kila sehemu katika wadi yangu ili wakaazi wa eneo hili wasiwe wanasumbuka kwa kukosa maji,” aliongeza Nyagaka.
Mwakilishi huyo pia aliahidi kufanya maendeleo zaidi katika wadi yake kabla ya uchaguzi ujao ili wakazi wa eneo hilo kufurahia matunda ya kumchagua kuwa kiongonzi.