Jamii imeshinikizwa kuzingatia msingi wa elimu bora mashinani na kuzuia kukithiri wa maswala ya itikadi kali miongoni mwa vijana wadogo ambayo husababisha ukosefu wa usalama katika kaunti ya Mombasa.
Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho amesema kwamba kuna haja ya wazazi kuwapa watoto wao msingi bora wa elimu, ili kumwezesha kujimudu katika siku za usoni.
Kulingana na Joho, wazazi wengi katika kaunti hiyo wamechangia pakubwa kwa vijana wao kujiunga na uhalifu, na kuvuruga usalama wa kaunti hiyo kutokana na kushindwa kuwajibikia majukumu yao kikamilifu.
Akiwahutubia wakazi wa mjini Mombasa siku ya Jumatano, Joho amesema kwamba kupitia kwa elimu bora hasa kuanzia elimu ya chekechea vijana wengi watafanikiwa kujitenga na baadhi ya watu flani walio na malengo ya kubadili fikra zao.
“Ni lazima wazazi kuwapata elimu bora watoto wao na kuwashauri kila uchao jinsi ya kujitenga na mswala ya itikadi kali kwani bila ya wazazi kufanya hivyo vijana wetu watajiunga na makundi hayo ya kihalifu na kuharibu usalama wetu,” alisema Joho.
Gavana Joho amewahimiza wazazi kuzingatia maswala ya elimu na kuwashauri watoto wao ili kuona kwamba kaunti ya Mombasa iko salama na kuwawezesha vijana kuzisaidia jamii zao katika siku za usoni.
Alisema kwamba kwa ushirikiano wa wazazi na viongozi wa kaunti hiyo, basi kaunti hiyo itaimarika kiusalama na kukuza uchumi wa kaunti ulisambaratika kutokana na misukosuko usalama kila uchao.
“Iwapo wazazi wataungana na kushirikiana kwa karibu mno na viongozi wa kaunti, basi usalama wa kaunti utaimarika na uchumi pia utakuwa kwa kasi,” aliongeza Joho.
Hata hivyo, kampeni ya kuwashuri vijana kujitenga na maswala ya itakadi kali na uhalifu inaendelezwa mashinani, na viongozi wa kaunti hiyo ili kuona kwamba kaunti ya Mombasa ni salama.