Vyama vya wazazi kutoka kaitka shule mbalimbali mjini Eldoret vimeelezea wasiwasi kuhusu uhalali wa mitihani ya kitaifa ya KSCE na KCPE mwaka huu.
Wazazi hao walisema kutokana na matukio ya kuwepo kwa wizi wa mitihani inayoendeela, itakuwa vigumu kubaini ufanisi wa watahiniwa katika mitihani husika.
Wazazi hao wametaka wadau wote kushirikiana ili kukabiliana na uhalifu wa wizi wa mitihani.
Wakihutubu Jumatatu wakati wa matembezi ya kukusanya fedha za kusaidia wanafunzi kutoka katika jamii maskini ambao wanaosomea katika shule ya Testimony mjini Eldoret wazazi hao walielezea kughadhabishwa kwao na ongezeko la wizi wa mitihani nchini.
Mwenyekiti wa chama cha wazazi katika shule hiyo Dkt Samuel Bwobengi alisema wakati umefika wa kubuniwa kwa sheria ambayo itaruhusu kuwepo kwa bodi za mitihani tafauti nchini.
“Tunahitaji kuwa na mashirika mbalimbali ya kutahini wanafunzi ambayo yatatoa mitihani ya viwango vya ubora unaohitajika badala ya kutegemea tu baraza la mitihani nchini KNEC.”
Kwa mujibu wa daktari Bwobengi ni kwamba baraza la mitihani nchini KNEC limeanza kushindwa na majukumu yake hivyo basi kuna haja ya kuwepo kwa shirika mbadala la kutahini wanafunzi.
Hata hivyo wazazi hao walipinga pendekezo la kusitisha mtihani husika mwaka huu kutokana na udanganyifu ambao unazidi kushuhudiwa.
“Makosa ya watu kadhaa hayawezi yakawa kigezo cha kutupilia mbali mtihani wote na kuadhibu hata waanfunzi wasiokuwa na hatia” alisema Bw Bwobengi
Msimamo huo uliungwa mkono na bi Susan Bett ambaye pia ni mwanachama wa chama cha wazazi Eldoret.
Bi Bett alitaka wadau wote na maafisa wakuu katika idara ya elimu na baraza la mitihani nchiniKNEC kuajibikia utepetevu huo.
“Sisi kama wazazi tumetekeleza wajibu wetu wa kulipa karo na kuwapa wanafunzi maziningira bora ya kusomea ni wajibu wa wakuu wa elimu kulinda mtihani wa kitaifa dhidi ya wizi”
Wazazi hao wanahisi kuwa wizi wa mithani husika unachangiwa na ufisadi ambao umekita mizizi katika taasisi mbali za uma.