Wazazi kutoka kaunti ya Mombasa wameitaka serikali kuhakikisha kuwa walimu wanalipwa mishahara yao na kutafuta suluhu la kudumu la migomo ya mara kwa mara ya walimu ili kusishuhudiwe mgomo mwingine kama huu uliofanyika na kuwaathiri wanafunzi hasa wale wanaoenda kufanya mitihani ya kitaifa.
Wazazi hao wametoa hofu yao kuwa huenda pia serikali ikakosa kuheshimu sheria hata baada ya walimu kunyenyekea na kusitisha mgomo kwa siku tisini, ambapo walimu wanahitajika kutafuta mwafaka baina ya vyama vya kutetea maslahi ya walimu na wawakilishi kutoka upande wa serikali.
Akiongea na mwandishi habari huyu siku ya Jumatatu, mwakilishi wa wazazi katika eneo la Mwembe Tayari mjini Mombasa, Swabrah Hassan alisema kuwa serikali imeonyesha mfano mbaya kwa wananchi pamoja na mashirika, ambapo itakuwa vigumu kwa baadhi ya watu kufuata sheria kutokana na serikali yenyewe kudharau uamuzi wa mahakama kuhusiana na nyongeza ya walimu.
Hassan alitaka kuwe na suluhu mara hii kwani migomo ya walimu imekuwa ikiwaathiri wazazi mno ikizingatiwa kuwa tayari wengine walikuwa washalipa hela za mahitaji pamoja na karo ilhali watoto wamekuwa nyumbani.
“Hatuna wakati wa kuendelea kushuhudia migomo mara mara kwa mara ilhali tunalipa pesa kama ushuru, serikali sharti izingatie sheria na kuacha kuwadhulumu walimu na wanafunzi kukosa elimu, ni haki ya mwanafunzi kupata elimu, na haki ya mwalimu kulipwa vizuri, hivyo tunaamini wakati huu serikali itapata suluhu la kutosha,” alisema Swabrah.
Hata hivyo alishukuru hatua ya walimu kuitikia amri ya mahakama na kurudi shuleni huku suala lao likitafutiwa mwelekeo wa kudumu.