Kamishna wa polisi katika Kaunti ya Mombasa amewataka wazazi kuwa makini katika malezi ya watoto wao na kuwajibikia mienendo yao kwa jumla, ili kuwaepusha vijana dhidi ya vikundi vya ugaidi na matumizi ya dawa za kulevya.
Kamishna huyo Nelson Marwa, alitoa wito huo hasa wakati huu ambapo vijana kutoka enea la Mombasa na kanda ya pwani kwa jumla, wamekuwa wakilengwa na makundi ya ugaidi kama al-Shabaab, ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi dhidi ya wakenya kwa kuwatumia wazawa kutoka Kenya.
Akiongea na waandishi wa habari kwenye ofisi yake siku ya Jumatano, Marwa alisema kuwa wazazi wana nafasi kubwa ya kuwaelekeza watoto wao na kubadilisha misimamo mibaya ambayo huenda wamekuwa nayo.
“Nawaonya vijana dhidi ya kujiingiza kwenye uraibu wa pombe na matumizi ya dawa za kulevya. Mkono wa serikali utawaandama na kuwashtaki kwa mujibu wa sheria kwenye katiba ya Kenya,” alisema Marwa.
Alisema kuwa serikali ya Kenya itaendelea kupiga vita vikali dhidi ya vijana waliopotoka na wahusika wakuu ambao wamekuwa wakiwauzia vijana dawa za kulevya.
Juhudi za kamishna huyo zimeshuhudia wengi wa vijana ambao walikuwa wamejiunga na makundi ya uharamia wakijisalimisha na asilimia kubwa kuridhia na kuanza kuishi maisha ya kawaida na kukiri kuwa waliweza kupotoshwa na rafiki zao.
Wazazi wengi kutoka mji huo wamesihi serikali kuu kwa ushurikiano na serikali ya kaunti kuwasaidia kuwapa wasia na ushauri maalum vijana kuachana na makundi kama hayo haramu.