Serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa ushirikiano na Chuo kikuu cha Kisii imeweka mikakati ili kuwapa wazima moto wa kaunti hiyo mafunzo ya kisasa.
Kulingana na afisa mkuu msimamizi wa huduma za umma kwenye kaunti hiyo Bw Vitalis Getange, serikali ya Kaunti ya Nyamira inajitayarisha kukabilia na visa vya moto siku za mbeleni.
"Serikali ya Kaunti ya Nyamira imo mbioni kuweka mikakati itakayo saidia kukabilia na mikasa ya moto kwa siku zijazo,” alisema Getange.
Getange alisema kuwa mafunzo hayo yatawapa maafisa hao ujuzi wa kisasa kuhusu matumizi mazuri ya mashine za kisasa ambazo zingali kununuliwa na serikali ya kaunti hiyo.
"Mafunzo tunayokusudia kuwapa wazima moto yatawasaidia maafisa hao kujua kutumia vizuri mashine hizo za kuzima moto ambazo zitanunuliwa na serikali ya kaunti ya Nyamira,” alisema Getenga.
Alisema kuwa ushirikiano huo unajiri baada yao kugundua kuwa wazima moto wanahitaji mafunzo zaidi yatakayo fanyika chuoni Kisii na kwenye afisi kuu za serikali ya Kaunti ya Nyamira.
Visa vya moto hasa katika shule, mikahawa na soko mbalimbali vimekuwa vikiongezeka hali iliyoilazimu serikali ya kaunti kuweka mikakati ya kuagiza gari za kuzima moto.