Share news tips with us here at Hivisasa

Kamati ya uhasibu wa fedha za umma katika bunge la kaunti ya Mombasa imemfanyia mahojiano ya kina Waziri wa fedha wa kaunti hiyo Hazel Koitaba kuhusiana na kupotea kwa shilingi milioni 496.

Mwenyekiti wa tume hiyo Fadhil Mwalimu amesema kwamba wamechukua hatua hiyo ili kubaini jinsi fedha hizo zilivyotumika, na iwapo waziri huyo atapatika na hatia, basi kama kamati watawasilisha mswada katika bunge la kaunti hiyo wa kumuondoa katika wizara hiyo.

Akizungumza na wahabari baada ya kikao hicho siku ya Jumatano, Fadhil alisema kwamba wanachunguza ripoti waliyopokea kutoka kwa waziri huyo pamoja na maafisa wengine wanne wa serikali ya kaunti hiyo kabla ya hatua dhidi yao kuchukuliwa.

“Kama kamati ya uhasibu wa fedha za umma kaunti ya Mombasa, tumemhoji waziri wa fedha wa kaunti hii na tumekusanya ripoti ambayo tutaichunguza, na endapo atapatikana na hatia, basi yeye pamoja na maafisa wengine wanne wa kaunti wataadhibiwa,” alisema Mwalimu.

Maafisa hao wanne ni Waziri huyo wa fedha, Katibu wa serikali ya kaunti hiyo, Karani wa Bunge la kaunti na aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya usambazaji maji.

Hii ni baada ya ripoti ya ukaguzi kutolewa na mkaguzi mkuu wa fedha za umma nchini Edward Onyango kwamba serikali ya kaunti ya Mombasa imetumia shilingi milioni 496 bila ya kuorodheshwa katika orodha za utumizi wa fedha za umma.