Wanaoendesha biashara ya hoteli kwenye kituo cha kibiashara cha Kisian Katika Kaunti ya Kisumu wameagizwa kuzingatia usafi wa wateja wao.
Wafanyibiashara hao wametakiwa kuhakikishia wateja usafi kwa kuwashonea wahudumu wao sare za kazi na pia kuwaidhinishia stakabadhi za kiafia kutoka Wizara ya Afya, mbali na kuboresha mazingira ya kazi kwa kuchimba mashimo ya kutupa taka.
Afisa wa afya wa eneo hilo, Bridget Ouma aliwaambia wafanyibiashara hao mnamo siku ya Jumatatu kwamba, ni sharti kuzingatia agizo hilo wakati huu ambapo serikali ya kaunti imewaonya wananchi kuhusu hatari za uwezekano wa mkurupuko wa kipindupindu katika Kaunti ya Kisumu.
Afisa huyo aliwaambia wafanyibiashara hao kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka kipindupindu eneo hilo ikiwa hali ya mazingira itasalia jinsi ilivyo kwa sasa.
Hali ya mazingira katika maeneo mengi ya kibiashara vitongojini mwa mji wa Kisumu huwa mbaya sana wakati mwingine hasa nyakati za mvua.
Awali mapema mwezi uliopita Wizara ya Afya mjini Kisumu ilitoa agizo kwa wamiliki wa nyumba za kupangisha mitaani kuchimba mashimo ya kutupa taka na vyoo.