Waendeshaji magari katika jiji la Mombasa wametakiwa kuwa makini wanapokua kazini, huku mvua nyingi ikitarajiwa kuanza mwezi huu wa kumi, kama njia moja ya kuepusha majanga na ajali kwenye barabara.
Akiongea siku ya Jumamosi na waandishi wa habari mjini Mombasa, kamishna wa kaunti hiyo Nelson Marwa alisema kuwa madereva wamekuwa na mazoea ya kupeleka magari kwa kasi hata wakati mvua imenyesha, hali ambayo alisema husababisha ajali.
Kamishna huyo alishauri madereva wote wa magari, wale wa tuktuk pamoja na wahudumu wa bodaboda wafuate sheria za trafiki, na kuwajibikia kazi na kukoma kutumia nafasi yao vibaya.
“Masharti na sheria za barabarani lazima zifuatwe na wahudumu wote wa magari na pikipiki pamoja na magari aina ya tuktuk ili kuepusha ajali ambazo huenda zikasababishwa na utelezi wa maji mengi ya mvua ambayo tayari inaanza katika msimu huu wa El Nino,” alisema kamanda huyo.
Aidha, aliwataka wale wanaotembea kwa miguu kuwa makini na kujiepusha kutembea karibu na barabarani kwani huenda magari mengine kujipata katika hali ya kuteleza na hata kuwagonga watu ambao wanatembea kando ya barabara.
Ushauri huu unatolewa siku mbili tu baada ya serikali kaunti ya Mombasa kwa ushirikano na idara zote husika na mambo ya majanga, ile ya hali ya anga, na idara nyingine kukutana na kutoa mwafaka na kuweka mikakati ambayo itakabiliana na janga hilo la El Nino.