Share news tips with us here at Hivisasa

Watu wanaotumia kivukio cha Likoni mjini Mombasa, wamelitaka shirika la huduma za feri kutenga maeneo maalum ya watu walio na mahitaji maalum pa kusubiria feri.

Hii ni badala ya kuwekwa kwenye pote moja na wengine ambao hawana changamoto za maumbile.

Akiongea Jumamosi kwenye kivukiohicho, Fatma Idi, ambaye ana changamoto za kimwili, alisema kuwa bado watu walio na ulemavu hasa wanaotumia vifaa vya kuwakimu kutembea hawajapewa nafasi hiyo.

Idi aliwapa changamoto wasimamizi wa shirika hilo la feri kuangazia suala hilo kwa dharura ili kina mama, walemavu pamoja na wazee kupewa heshima. Aliongeza kuwa watu sampuli hiyo hujipata pabaya hasa nyakati za haraka ambapo kunazuka msongamano wa watu ambao mara si moja umesababisha maafa kwenye kivukio hicho.

Laula Mwambi, mama mwenye miaka zaidi ya sitini na tano, alisimulia jinsi watu wengi walio na umri kama yeye wanavyojipata taabani kwa kusukumwa ambapo walio wanyonge huanguka na kukanyagwa hata kuaga dunia.

Mama huyo ambaye hutumia kivukio hicho mara kwa mara alisema kuwa sharti serikali ya kaunti ya Mombasa kuingilia kati ili kuwaepusha na janga baya.

"Sisi hapa si ngombe wala mbuzi. Twaomba shirika hili la feri hapa Mombasa kuamka kutoka usingizi na kutatua janga hili ambalo linawakodolea macho," alisema Mwambi.

Mmoja wa maafisa wa shirika hilo ambaye hakutaka kutajwa alisema kuwa hivi karibuni, shirika hilo litashughulikiwa kilio cha abiria hao.