Wakulima na wafugaji wa mifugo kutoka kaunti ya Nyamira wameiomba serikali hiyo kupitia sekta ya Kilimo kutoa mafunzo ya kilimo kama njia moja ya kuinua viwango vya kilimo.
Wakiongea siku ya Jumatano katika kijiji cha Boyagesimo, wadi ya Gesima wakati wa kupokea mafunzo ya Kilimo kutoka kwa wahisani wema, wakaazi hao walisema kuwa mafunzo yanahitajika pakubwa ili kuinua viwango vya maendeleo.
Kwa sasa wakulima hao wameiomba sekta ya kilimo katika kaunti ya Nyamira kuandaa mikutano ya mafunzo ili wakulima hao waweze kupata mbinu mpya za kilimo.
“Tunaomba sekta ya kilimo katika kaunti ya Nyamira kutuandalia mikutano ya mafunzo ili nasi tuweze kupata kufunzwa mbinu mpya za Kilimo,”alihoji Kiage Edward, Mkulima.
Kulingana na wakulima hao, hawajafaidika pakubwa na sekta ya kilimo kama vile kupokezwa mbolea kama kaunti zingine, huku wakiomba waziri wa kilimo kushughulikia masuala ya kilimo na kuwakumbuka wakulima.
Aidha, waliwapongeza wahisani hao kutoka Rigoma kwa kujitolea na kutoa mafunzo hayo, na kuomba serikali ya kaunti ya Nyamira kuiga mfano huo na kusaidia wahisani kama hao hili waweze kufikia wakulima wote.
Baadhi ya mafunzo waliyopata ni jinsi ya kufuga Kuku, sungura, mbuzi na ng’ombe, na pia jinsi ya kupanda mimea na kutunza mimea mbali mbali.
“Napongeza wahisani hawa kwa kujitolea kutoa mafunzo ambayo ni faida kubwa kwetu kama Wakulima,” alihoji Rodgers Ondieki, mkaazi.