Utafiti uliyofanywa na Shirika la ‘Amnesty International Kenya’ umebaini kuwa zaidi ya familia 100 kutoka eneo zima la pwani huvunjiwa nyumba zao kila mwaka bila notisi, na kuachwa bila ya makao licha ya serikali kulitambua hilo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne baada ya kuzindua ripoti ya utafiti uliyofanywa na shirika hilo kwa muda wa miaka mitatu, Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Justus Nyang’aya alisema kwamba hatua hiyo imechangia kukithiri kwa migogoro ya ardhi kila uchao, huku wengine wakijitosa katika maswala ya kihalifu.
Nyang’aya amesema kwamba iwapo serikali ama viongozi mbalimbali pamoja na wawekezaji wanataka kutumia ardhi za wakazi kwa maswala ya kimaendeleo, basi lazima kushauriana na wamiliki wa ardhi hizo na hata kuwalipa fidia kabla ya kuwafurusha ili kutekeleza miradi katika ardhi hizo.
“Serikali ama viongozi wowote wanaotaka kutumia ardhi za wakazi kwa ajili ya kufanya miradi ya kimaendeleo ni lazima iwajulishe wakazi kwa mazungumzo iwapo watakubali basi wapewe fidia na wapelekwe katika ardhi wazilizotengewa,” alisema Nyang’aya.
Wakati huo huo, ameikosoa serikali kwa kuwafurusha wakazi wa eneo la Dunga Unuse katika eneo bunge la Changamwe na wale wa Jomvu kwa ajili ya miradi ya kiserikali na ya kibinfasi, akisema kwamba hatua iliyochukuliwa kuwafurusha wakazi ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na katiba ya nchi.
Mwanaharakati huyo ametoa shinikizo kwa serikali kuzingatia haki za kibinadamu kabla ya kufanya uamuzi wowote wa kuwafurusha wakazi na akasema kwamba iwapo swala hilo halitazingatiwa, huenda kukashuhudiwa mgawanyiko mkubwa wa wakazi kutokana na mizozo ya ardhi.