Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Zaidi ya familia 400 kutoka kijiji cha Nguu Tatu, eneo la Kisauni, mjini Mombasa, wamefurushwa katika makazi yao na bwanyenye mmoja anayedai kuwa ardhi hiyo ya hekari 600 wanayoishi wakazi hao kuwa yake.

Mzozo huyo wa ardhi ulikuwa umesitisha na mahakama baada ya wakazi hao kuwasilisha kesi mahakamani wakilalamikia kufurushwa katika ardhi hiyo wanayodai kuishi kwa zaidi ya miaka 40.

Wakizungumza siku ya Jumtatu, wakazi hao wakiongozwa na Martin Chiponda walidai kwamba bwanyenye huyo kwa jina Mahmoud Hussein alikodisha vijana pamoja na maafisa wa polisi wakusimamia vijana hao kuwafurusha wakazi hao katika ardhi hiyo pamoja na kuwavunjia nyumba zao huku zingine zikichomwa.

“Hatua ambayo bwanyenye huyo amechukua ya kutuvunjia makazi yetu na zengine zikichomwa ni makosa makubwa kwa sababu tayari tuko na barua ya kuishi mahali hapa kutoka kwa mahakama. Lakini kwa kuwa yeye ana pesa, basi ametumia nguvu zake kutufurusha mahali hapa. Sisi hatuende kokote hadi pale serikali itakapoingilia kati swala hili na kulitatua,” alisema Chiponda.

Chiponda aliishtumu Tume ya kitaifa ya ardhi nchini NLC kwa kushindwa kuingilia kati mgogoro huo na kuwasaidia wakazi hao licha ya wao kuwasilisha lalama zao, huku akisema kwamba zaidi ya vijana 13 kutoka eneo hilo wametiwa nguvuni na maafisa wa polisi kwa madai ya kuzua vurugu.

Hapo awali mahakama ya mjini Mombasa ilisitisha kufurushwa kwa wakazi hao na bwanyenye huyo aliyedai kuwa jamii inayoishi katika ardhi hiyo wameanza kutaka vipande vya ardhi na kuviuza kwa shilingi elfu tano na elfu 10 kinyume na jinsi mahakama ilivyo agiza.

Kwa sasa wakazi hao wameitaka serikali kuingilia kati swala hilo kwa kuwa hawana mahali pa kwenda na vifaa kwa kujisaidia kwani nyumba zao zimevunjwa na kuteketezwa.