Zaidi ya vijana hamsini wametiwa mbaroni kwa kuzua fujo na kuharibu mali na kuchoma magari katika eneo la Tudor baada ya wanafunzi wa chuo cha ufundi cha Mombasa kuzua ghasia kwa madai kuwa chuo hicho kimeongeza karo bila ufahamu wa usimamizi wa viongozi wa wanafunzi wa chuo hicho.
Asilimia tisini walioshikwa ni wanafunzi wa chuo hicho, na baadhi ya wengine ni vijana wa mtaa ambao walionekana kuaharibu na kuporwa mali na kuchoma magari ya watu nje ya lango kuu la kuelekea chuo hicho na barabara kuu ya kutoka Tudor kuenda mjini Mombasa.
Kulingana na afisa mmoja wa kupambana na ghasia ambaye aliongoza maafisa wenzake katika operesheni ya kutuliza hali hiyo, wengi waliokamatwa na maafisa wa polisi ni vijana wa kiume na idadi kama sita walikuwa wasichana na wengi wa washukiwa hao ni wanafunzi kutoka chuo hicho cha Kiufundi cha Mombasa (TUM).
Afisaa huyo aliongeza kusema kuwa wanafunzi hao pamoja na vijana wengine wa mtaa walioshirikiana nao watazuiliwa na watapelekwa mahakamani siku ya Jumatano na kufunguliwa mashtaka ya kushiriki uhalifu na kuzua fujo ambazo zimesababisha kuchomwa kwa mali ya watu.
Wanafunzi hao walizua ghasia baada ya madai kuzuka kuwa chuo hicho kimeongeza karo bila kuwafahamisha wanafunzi, na chuo hicho kilifungwa rasmi na mamlaka ya chuo na wanafunzi kutakiwa kuenda nyumbani hadi watakapojulishwa.