Zaidi ya wanawake 4,100 kutoka eneo bunge la Nakuru Mashariki, Kaunti ya Nakuru, wamefaidi kutokana na pesa za hazina ya maendeleo ya wanawake, almaarufu kama 'Women Enterprise Fund'.
Afisa anayesimamia hazina hiyo, Violet Nyairo, amesema kwamba zaidi ya Sh43.3m zimepewa wanawake hao kama mkopo.
Nyairo amepongeza hatua ya kujitokeza kwa wanawake hao waliyo katika vikundi 412.
Nyairo aliyekuwa akizungumza na wanahabari mjini Nakuru siku ya Alhamisi alisema lengo la pesa hizo ni kuinua na kuboresha hali ya maisha ya wanawake kutoka eneo bunge hilo.
Aliongezea ya kwamba tangu mwaka wa 2007 hadi wa sasa, zaidi ya Sh250m zimepewa wanawake kama mkopo.
“Wanawake wamekuwa wakiachwa nyuma kimaendeleo kwa muda mrefu, hali ambayo ni sababu kuu ya wanawake wengi humu nchini kukumbwa na ufukara,” alisema Nyairo.
Nyairo alitilia mkazo kwa wanawake zaidi wajitokeze na kujiunga na vikundi vya watu kumi, wasajiliwe ili waweze kupewa pesa za kuendeleza kazi au biashara zao, bila kulipia riba yoyote wanaporejesha mikopo hiyo.
Hata hivyo, Nyairo amevihimiza vikundi vilivyopewa mikopo hapo awali wafanye bidii na kulipa pesa hizo..