Share news tips with us here at Hivisasa

Jamii ya watu wanaoishi na ulemavu Pwani wameitaka idara ya usalama kuwachunguza walanguzi wa dawa za kulevya wanaotumia jamii hizo kuuza mihadarati na wafunguliwe mashtaka.

Kulingana na mshirikishi mkuu wa jamii hiyo Pwani Hamisa Zaja, walanguzi wa mihadarati wamekuwa wakiitumia jamii hiyo katika kujibinafsisha wenyewe na kuicha jamii hiyo katika hali ngumu ya kukabiliana na maafisa wa usalama pasi na kujua hatima yao.

Akizungumza na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumamosi,  Zaja amesema kwamba iwapo maafisa wa usalama watazuru hadi mashinani kuwachunguza walanguzi hao na kuisaidia jamii hiyo kushurutishwa kutekeleza biashara hiyo haramu bila hiari yao basi jamii hiyo itakuwa na amani.

“Tumeona mara nyingi vijana wanaoshikwa na maafisa wa polisi wakiuza na kutusamba dawa hizo ni walemavu. Sasa ndio sisi twasema kuwa lazima walanguzi wachunguzwe na washikwe kisha wafunguliwe mashtaka. Walemavu kutekeleza jambo hili sio kupenda kwao wanalazimshwa,” alisema Zaja.

Zaja amewataka maafisa wa usalama kufanya uchunguzi wa kina ili hatua kali dhidi ya walanguzi hao ichukuliwe ili kusitisha kuenea kwa biashara hiyo haramu iliyowapotosha vijana wengi wa umri mdogo.

Wakati uo huo ameunga mkono hatua ya maafisa wa usalama dhidi ya uparesheni ya kuwasaka walanguzi na watumizi wa dawa za kelevya hapa Pwani akisema kwamba hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa kuenea kwa biashara hiyo.