Harambee Stars wameruka juu ya jedwali la kundi F baada ya kutoka sare tasa na Ethiopia kwenye mechi ya kufuzu kombe la AFCON, iliyochezwa Jumatano, katika uga wa kitaifa, Bahir Dar.
Sare hiyo imetunuku Kenya pointi moja na kuizolea alama 4 kwa mechi mbili, sawa na Uhabeshi japo Stars wana ubora wa mabao.
Kenya na Uhabeshi watacheza mechi ya marudiano Jumapili, katika uwanja wa kimataifa wa MISC, Kasarani.
Jinsi hali ilivyo kuwa katika kipindi cha kwanza
Timu zote zilikosa makali kwenye safu ya ushambulizi katika kipindi cha kwanza. Huku Uhabeshi ikipata nafasi zaidi za kufunga ikilinganishwa na Kenya.
Hata hivyo safu ya ulinzi ya Stars ilisimama tisti na kuwalazimu wenyeji kupiga mashuti ya mbali; juhudi amabazo hazikuzalisha matunda.
Mshambulizi Getaneh Kebede alikuwa mwiba kwa mabeki wa Kenya na karibu afunge hata hivyo shuti lake lililenga kando ya lango.
Pia Stars walizalisha nafasi kadha za kufunga walakini, hawakuweza kuzitumia vilivyo, huku nahodha Victor Wanyama akipoteza nafasi ya wazi kunako dakika ya 40, kwani alilenga shoti lake kwa mikono ya kipa Asefa, ambaye alizima shambulizi hili bila wasiwasi.
Wahebeshi wazidisha mashambulizi Kipindi cha pili
Uhabeshi walizidisha mashambulizi baada ya kurejea kwa kipindi cha pili, hata hivyo ngome ya Stars iliwadhibiti vilivyo na kuonekana kuwazidi maarifa.
Huku muda ukiyoyoma, kipa Patrick Matasi alizima tumaini la nguvu mpya Omod Okwury kwa kuokoa mkwaju wake baada ya kupenya kwenye eneo la hatari.Winga Paul Were aliongeza nguvu mpya kwa Stars baada ya kuingia dakika ya 74, na kuwapa wakati mgumu difensi ya Uhabeshi, hata hivyo sawa na wenzake pia naye alipoteza nafasi ya kuiweka Kenya mbele.
Na Refa Bakary Papa Gassama alipopuliza kipenga cha mwisho mambo yalisalia kuwa sare tasa. na kazi ipo kwa Kenya, haswa Jumapili wanapoalika Uhabeshi, kwenye kidumbwedumbwe ambacho lazima wazoe alama zote tatu iwapo wanahitaji kucheza katika kipute cha Afcon, kule Yaounde, Cameroon.
Vilevile, kibarua kipo kwa mashabiki kuweza kujitokeza na kuzidi wahebeshi kwa kujaza uwanja wa Kasarani ujae hadi ufurike furi furi.