Idadi kubwa ya wananchi katika kaunti za Kisumu na Isiolo, hawana ufahamu mwafaka kuhusu wadhifa wa Useneta na mwakilishi wa wanawake.
Hii ni kulingana na matokeo ya utafiti, uliofanywa na Shirika moja liitwalo Wel-read Initiative.
Utafiti huo uliofanywa hivi maajuzi, unaonesha kuwa wananchi wengi katika Kaunti hizo wanafahamu vyema nafasi za gavana na mwakilishi wa wadi, kwa sababu afisi zao ziko mashinani.
Akizungumza jijini Kisumu mapema Jumatatu wakati akizindua ripoti ya utafiti huo, afisa mkuu wa shirika la Wel-read Initiative Hesbon Ouma, alisema kuwa utafiti huo vile vile ulibaini kuwa asilimia kubwa ya wananchi hupata ujumbe kuhusu maswala ya Kaunti kupitia vyombo vya habari, huku redio ikiongoza kwa asilimia 31.
“Kwa mfano tuliwauliza baadhi ya wale tuliowahoji kuhusu nafasi za uongozi katika taifa hili, wengi wao walitaja nafasi zote isipokuwa nafasi ya mwakilishi wa wanawake na Seneta,” alisema Ouma.
Kwa upande wake, afisa mpanga ratiba wa mashirika ya kijamii jijini Kisumu Betty Okero, alizihimiza serikali za kaunti kushirikiana na mashirika ya kijamii, ili kuwawezesha wananchi kuhusishwa kikamilifu kwenye maswala ya bajeti na mipango ya maendeleo.
Kulingana na katibu, jumla ya viongozi sita wanafaa kuchaguliwa kwenye kila uchaguzi mkuu.
Viongozi hao ni Rais, Gavana, Seneta, mwakilishi wa wanawake katika kila Kaunti, Mbunge na mwakilishi wa wadi.